SAUTI YA MALENGA, SI WENZETU HAWA WATU

Tulidhani ni wenzetu, wakombozi wa taifa
Tukawapa kura zetu, kwazo wazizibe nyufa
Kumbe walaji wa watu, watufyonza hadi twafa
Si wenzetu hawa watu, viongozi wana kutu

Wanaranda kwa siasa, nzige wanapotufyonza
Wapo Nyeri na Mombasa, BBI wakifunza
Ghalibu wanatuposa, ni lini tutajifunza
Si wenzetu hawa watu, viongozi wana kutu

Magavana wafujaji, hela zetu wanafuja
Isitoshe na majaji, wamengia kundi moja
Raia hawana maji, iweje mvikwe koja
Si wenzetu hawa watu, viongozi wana kutu

Kuna wale wa sakata, hazina wameziponza
Kisha watajatakata, ‘uzalendo’ watatunza
Watuchezea karata, huku damu watufyonza
Si wenzetu hawa watu, viongozi wana kutu

ALSO READ:  KWETU WAPO

Jicho huku wamefumba, lipo janga la kutisha
Duniya yote yayumba, korona sasa yabisha
Tusije kunuka vumba, wongozi ukitufisha
Si wenzetu hawa watu, viongozi wana kutu

Wazalendo zindukeni, mambo haya hatuhusu
Hongo, rushwa kataeni, komeni kupigwa busu
Na maovu yasemeni, tusikumbatie lusu
Si wenzetu hawa watu, viongozi wana kutu

Kaditama namaliza, nashitakia kwa Mungu
Haya yanayoniliza, na kunitiya machungu
Na sauti tutapaza, kuyaondoa magugu
Si wenzetu hawa watu, viongozi wana kutu

Share this

Leave a Reply

Your email address will not be published.