SHAIRI LA WIKI.

SAUTI YA HAKI: WACHENI DHULUMA POLISI.

Usalama mwadumisha, ndo jukumu la kazi.
Dhuluma iwe la hasha, pambaneni na wizi.
Mateso mwawapasha, wengine ni wazazi.
Sheria inasema, wacheni dhuluma polisi.

Boresheni usalama, amani umoja pendo.
Zipo nyingi lalama, mmekwenda hasa kando.
Heshimuni kina mama, waliwabeba na chondo.
Sheria inasema, wacheni dhuluma polisi.

Maisha wamepoteza, wengine waso dosari.
Wazazi mara kuwaza, dhuluma ndio hatari.
Firimbi washapuliza, nikaandika shairi.
Sheria inasema, wacheni dhuluma polisi.

Sio nyote narudia, wapo wale wangwana.
Yapo mazuri twasikia, fahamuni twaona.
Wengine husaidia, ni jambo lakufana.
Sheria inasema, wacheni dhuluma polisi.

ALSO READ:  JOSEPHAT LAKA: NITOE GEREZANI

Rungu mkitumia, msiwavunje mifupa.
Utulivu mliapia, kiapo nacho mkaapa.
Kuwalinda raia, sio kuwavunja makwapa.
Sheria inasema, wacheni dhuluma polisi.

Toa chozi kitumia, sifuatishe yo risasi.
Wamehaidi kutulia, kutibuka so rahisi.
Sio kwamba natetea, wakamatwe waasi.
Sheria inasema, wacheni dhuluma polisi.

Kazi yenu tavutia, kiifanya kwa usawa.
Sifa tawamiminia, kwa furaha maridhawa.
Mara tena narudia, sio pauka pakawa.
Sheria inasema, wacheni dhuluma polisi.

Ndio hivi kumalizia, natumai mewafikia.
Nenda zangu kutulia, bakini mkiwazia.
Kwa pole mewandikia, si kwamba napapia.
Sheria inasema, wacheni dhuluma polisi.

Avatar
Josphat Laka
Josphat Laka is a third year student at EGERTON UNIVERSITY taking bachelor of PROCUREMENT AND SUPPLY CHAIN MANAGEMENT, a freelancer and a poet.
http://aowapress24.com

Leave a Reply

Your email address will not be published.