HEALTH LIFESTYLE POEM

SHAIRI : MENO KIJANI

Kwa weledi napekua, na kunena hadharani.
Wengi wao tajutia, kutafuna yo majani.
Bora hasa kufikiria, na kutazama usoni.
Meno yao kijani, ati miraa starehe!

Wamejaa kotekote, vikundini tawakuta.
Basi huu ni upwete, miti hii ni matata.
Ombi lao ni wapate, hawajui watajuta.
Meno yao kijani, ati miraa starehe!

Wamejaza mifukoni, miraa ati ni raha.
Yafikie sikioni, ikizidi ni karaha.
Waongea kwa utani, wakidhani ni mzaha.
Meno yao kijani, ati miraa starehe!

Imewafilisi wengi, wamebaki ombaomba.
Hasara nazo ni nyingi, kimo chake kama mwamba.
Walonavyo hawaringi, ndio hivi mimi namba.
Meno yao kijani, ati miraa starehe!

ALSO READ:  BRENDA HOLO: An insight on African village life.

Zipo nyingi zo hatari, kutolala ndiyo mosi.
Heri hasa taadhari, toa huu wasiwasi.
Funga yako yo safari, jinasue kadamnasi.
Meno yao kijani, ati miraa starehe!

Mipango yao bandia, ukiwazia taswira.
Midomoni hubugia, maatawi kwa papara.
Ukichimbua hatua,wengi wao huhara.
Meno yao kijani, ati miraa starehe!

Uchafu ni nembo yao, harufu itakujuza.
Ni kero kwa wakezao, na watoto huwaliza.
Afadhali vipepeo, angalau wapendeza.
Meno yao kijani, ati miraa starehe!

Sio kwamba nina chuki, kazi yangu kwelimisha.
Mengi ng’o hayasemeki, zingatiya lowapasha.
Ukijawa na hamaki, tema chini itawasha.
Meno yao kijani, ati miraa starehe.

Avatar
Josphat Laka
Josphat Laka is a third year student at EGERTON UNIVERSITY taking bachelor of PROCUREMENT AND SUPPLY CHAIN MANAGEMENT, a freelancer and a poet.
http://aowapress24.com

Leave a Reply

Your email address will not be published.